Knowledge

IFAHAMU DOMINIKA YA MATAWI.

Jumapili ya matawi ni jumapili moja kabla ya sherehe ya Pasakabambayo kwa mujibu wa Injili, Kanisa Katoliki huanza wiki takatifu kwa lengo la kukumbuka mateso, kifo na ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo.
Pia ndiyo siku maalumu ambayo Wakristo wengi hukumbuka na kusherekea siku ile Yesu alipoingia Yerusalemu kwa mara ya mwisho kama Mwokozi na Mfalme wao.
Inasemekana kuwa, siku hiyo Yesu alipokuwa anaingia Yerusalemu alipanda punda huku umati mkubwa wa watu hasa vijana wakimfuata kwa furaha, wengine walishika matawi na kutandaza nguo zao chini ili kumpa Yesu heshima ya Kifalme na kuimba:
Hosana Mwana wa Daudi, ndiye Mbarikiwa, yeye ajaye kwa jina la bwana, hosana juu mbinguni. (Mathayo 21:1-11)
Neno la Mungu linatuambia kwamba, tukio hilo la kupunga matawi na mengine kuyatandaza chini ili Yesu apite juu yake, basi matawi hayo yaliwakilisha mema na alama kubwa ya ushindi juu ya kifo alichokishinda Yesu baada ya siku tatu alipofufuka kaburini. (1Wakorintho 15:55)
Lakini pia kitendo cha Yesu kupanda punda, ilikuwa ni kutimiza ule unabii uliotolewa tangu kale juu ya ufalme wake, maana nyakati zile Wafalme wa Kisraeli walipokuwa wakilakiwa na watu huwa wanapanda punda, huku wakiimbia nyimbo za kishujaa.
Kibiblia Punda huwakilisha amani, kwahiyo wale waliomlaki Yesu, walionesha kujawa na amani, kwa kuwa walimuona Yesu kama Mfalme wao atakayeleta amani ndani ya taifa la Israeli. (Zekaria 9:9)
Kadhalika hata neno Hosana Kibiblia lilimaanisha Okoa sasa, hivyo Waisraeli walimwiimbia Yesu wimbo huo wakiamini kwamba, muda si mrefu yule Masiha waliomgojea ataenda kuwaokoa dhidi ya ukatili, manyanyaso na dhuluma ya dola ya kirumi iliyokuwa inatawala nchi yao.
Ingawa Biblia inafunua wazi kuwa, japo Waisraeli walimuona Yesu kama Mfalme wao kwenye mambo ya siasa, kumbe Yesu hakuja ulimwenguni kwa ajili hiyo, bali alikuja ili kutuokoa kutoka kwenye dhambi ya mauti na kifo, na hiyo ndiyo ilikuwa ajenda kuu ya utume wake alioufanya hapa duniani miaka 2000 iliyopita. (Yohane 12:12-15, Zaburi 118:25-28 na Warumi 10:9)
Pia hata Yesu alipokuwa anaukaribia mji, Biblia inatuambia kwamba aliulilia sana kwa machozi licha ya kushangiliwa kwa furaha na watu waliomzunguka. Maana alitambua kuwa, muda si mrefu wale wanaomshangilia ndio watakaomsaliti na kumuua kwa kifo cha aibu na maumivu makali pale Msalabani Kalvari. (Luka 19:41-42)
Hivyo nihitimishe kwa kusema kwamba, jumapili hii ya matawi itukumbushe kufahamu kuwa Yesu Kristo ndiye Mkuu kuliko mtu yeyote yule duniani, na hii ndiyo sababu kuu ya kusherekea juma hili, kwani kupitia sadaka ya kifo chake pale Msalabani, sote tuliwekwa huru kutoka mauti na kuingizwa kwenye furaha ya uzima wa milele.
Basi ndugu zangu Yesu tunayemshangilia leo, tukamshangilie siku zote katika maisha yetu kwa kutenda mema na kuacha maovu wala tusimsaliti kama vile Waisraeli walivyofanya, bali tuwe waaminifu kwa Mungu na jirani zetu, maana usaliti sio mzuri, inaweza kuondoa amani na kuleta machafuko pamoja na mauaji kwa wale wanaotuamini, hivyo tujifunze kupitia tukio hili la matawi ili tuishi vizuri na wenzetu
Asante na Mungu awabariki

"During these 40 days, let me put away all my pride. Let me change my heart and give up all that is not good within me. Let me love God with all that I am and all that I have." —Genesis Grain.